Ngonjera

Ngonjera ni aina ya mashairi ya majibizano baina ya pande / watu wawili au zaidi. Muundo ni sawa kabisa na mashairi. Isipokuwa, katika muundo huo, majina ya wahusika yanaongezwa kama kwenye tamthilia.
Aghalabu mazungumzo hayo huwa na mijadala ya malumbano yenye kusudio la kutoa ujumbe maalumu kwa hadhira au jamii husika. Msemaji mmoja huuliza swali katika ubeti mmoja na mwingine hutoa jibu katika ubeti unaofuata na majibizano ya hoja kuendelea hivyo hadi kukamilisha mada ya mjadala husika. Kutokana na sifa hiyo, ndiyo maana kipera cha ngonjera kinapatikana katika utanzu wa ushairi na katika utanzu wa maagizo.
Aina hii ya mashairi ilibuniwa na mshairi maarufu Tanzania Mathias Mnyampala. [1][2] Neno lenyewe la 'ngonjera' ni neno kutoka lugha ya Kigogo, kabila lake Mathias Mnyampala, linalomaanisha 'kubisha' au 'ubishi'[3]. Katika jamii ya kijadi ya Wagogo, ngonjera ni malumbano ambapo watu wanabishana mpaka wapate suluhisho la mambo fulani kama mahari au sababu ya kifo cha mtu. Utaratibu huo unaonekana kwenye Ngonjera za kishairi za Mnyampala ambapo watu wanabishana mpaka watambue kuwa siasa ya Ujamaa ni sawa kabisa. Kwenye lugha ya Kiswahili maana yake imegeuka kidogo kumaanisha "kwenda pamoja" au "kutembea kwa pamoja"[2] ila maana hiyo pia inabeba fikira ya utaratibu wa kijamii wa usuluhishi (uwe wa kweli au wa kubuniwa kwenye mashairi) unaolenga kupata suluhisho la mambo maalumu kupitia malumbano.
Tanbihi
- ↑ "Mathias Eugen Mnyampala". Mwananchi. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-01-26. Iliwekwa mnamo 2020-01-26.
- 1 2 Mulokozi, Mugyabuso M.; Sengo, Tigiti S. Y. (1995). History of Kiswahili Poetry, A.D. 1000-2000: A Report (kwa Kiingereza). Institute of Kiswahili Research, University of Dar es Salaam. ISBN 978-9976-911-22-0.
- ↑ Charles M. Mnyampala na Mathieu Roy. About the meaning of the word 'ngonjera' from Cigogo in Kiswahili - Part 1. 2011. ⟨medihal-01121445v2⟩ Part 2. 2011. ⟨medihal-01121451v2⟩ Part 3. Fieldwork in Ugogo (Tanzania). 2011. ⟨hal-04535582⟩
| Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ngonjera kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |